Villagers of South Unguja Pete acquiring knowledge about the fight against AIDS through Jihadhari magazine released by Zanzibar AIDS Commission
Children at ZAPHA+
ZAC Monitoring and Evaluation Coordinator Mr. Ali Kimwaga in one of the M&E meeting
Theatre for Social Development (THESODE) on the stage
Group Picture during World AIDS day climax 2015
Participants attended National Youth Forum in Zanzibar
Group Picture during World AIDS day climax, 1 December 2016
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud Mohamed akizungumza na Watendaji wa Wizara yake ikiwemo Tume ya UKIMWI ambayo imehamishiwa Wizara hiyo.

ZAC Chairperson

Welcome to the Zanzibar AIDS Commission (ZAC) Website. We hope that the ZAC website will serve to give a closer picture about ZAC...Read More

Kutoka Mwanajeshi, dawa za kulevya hadi Meneja wa Sober House.  

Pengine   sasa hivi angalikua  amevaa gwanda, asubuhi  gwaride;  huu haaa huu   haap,   na mchana kwenye kikosi cha mizinga, dush !  dush! Gishaaa !

Anakumbuka  hata alikua anajua kutegua  mzinga wa aina gani;  ni  85  mzinga maalum   wa kupiga kama vile   ngome, magorofa  au hata  meli  za  adui. Lakini  mabonde ya safari ya  maisha yalimpoteza kabisa kwani alifukuzwa jeshini  na kupoteza haki zake  zote, alifungwa   kwa  miaka mitatu na  baadae  miezi mitatu kwa makosa  ya kuvunja na  kuiba. Lakini sasa yeye anasema ni  zaidi ya  milionea, ana utajiri  mkubwa katika maisha yake.  “Si utajiri  wa fedha wala  mali  bali ni utajiri   wa kuishi kwa furaha bila ya kutumia  dawa  za kulevya, kwani ndio iliyoniharibia maisha yangu ‘’

Anasema  Moh’d  Kassim Iddi  maarufu Chatu. 

Aliponiambia kwa utani  anaitwa chatu, nilishituka sana. Chatu ni miongoni mwa majoka makubwa na ya  hatari, anaweza kumeza  hata  mbuzi na vengine  visivyomezeka. 

‘’Kwa  nini wanakuita Chatu  na unakubali?’’  Nilimuuliza, 

‘’Aaa  hilo  ni jina  la umaarufu wangu nilipokua  jeshini. Enzi  hizo  nilikua nasifika kwa utoro. Naweza kuchomoka hata kwenye gwaride na usijue nimeenda wapi. Nilikua  na tabia  ya  mkono mkono kwani  nilishaanza kupasha kama vile  bangi,  pombe na dawa  nyengine za kulevya’’  Aliniambia.

Tabia yangu ya kunyererekeka nyerereka kama  nyoka  ndio  masela wakaniita  ‘Chatu!’   alisema  huku akicheka.  

Nilishituka sana baada ya kutajiwa baadhi ya vijimambo vinavyopatikana jeshini. Nilipomuuliza  sana  alisema, ‘’ Aaa bro  mengine yawache  tu, mambo ya watu, ya  kawaida  tu  kwa   mazingira  ya vikosi ’’Alijibu akicheka.

Yaliyomsibu   Chatu yanaweza kumsibu kijana yeyote katika maisha. Anahadithia kwamba mnamo mwaka 1990 aliajiriwa na  jeshi  la  wananchi wa Tanzania wakati huo akiwa na umri wa  miaka  18.  Kijana mbichi  mwenye nguvu kwa sasa  unaweza kusema sharobaro. Maisha ya jeshini anasimulia yana  mambo mengi. Marafiki wenye tabia ya  kila  aina na wanaotoka  katika  maeneo  tofauti ya Tanzania .

‘’Nilijichanganya tu nawashkaji. Nilianza na  sigara  ndogo na  baadae  sigara kubwa, nikaanza kupiga kikombe cha babu (bia)    na  baadae mambo fulani. Si unajua mwisho wa mwezi kikieleweka hapatoshi’’. Anasimulia  Moh’d ambae alikuwa katika  kikosi cha mizinga hapo Ali Khamis Camp Vitongoji. 

Miaka   kumi  na  nane  ya jeshini anasimulia Moh’d kwake hayakua ni ya ulinzi wala usalama  kwa wananchi. Lakini ilikua uhasama na wananchi na wanajeshi wenziwe.

‘’Nakumbuka nishaadihibiwa mara kibao kwa makosa ya kinidhamu. Mara  nimeiba cha huyu, paredi sionekani, nalala mtaani. Wakati mwengine siku  tatu hadi nne  sijaingia jeshini. Nilikua  naingia  mitaani kutafuta madawa ya kulevya  na  kupasha’’. Anasimulia  Moh’d.

Waswahili wanasema mwizi  ana arobaini zake. Ilipofika  mwaka  baada ya kulitumikia jeshi kwa  muda wa  miaka 13 tokea  mwaka  1990  hadi  2002. Uongozi wa  jeshi  hilo ulichoshwa na  visa  vya Moh’d  au chatu, alikua keshameza mengi. Na alifukuzwa  rasmi na kupoteza haki  zake zote  kama mtumishi. 

Anasimulia kwamba, ‘’Wala sikujali, sababu sikuwa na akili yangu, nilikua na akili nyengine kwani  madawa ya kulevya yalishanipiga  vibaya; kimwili  na kiakili. Nilikua choka mbaya ‘’ Anasimulia Moh’d  na kujutia  hayo aliyoyatenda. 

Mbona kichaa  alipewa rungu! Mara  tu baada ya kutoka uzio wa kambi  ya  jeshi basi ndivyo  chatu akawa chatu kweli. Aliingia  mtaani na kuaza kumeza vya  watu; penye nguo iliyoanikwa,  kuku, simu, waya wa dirisha na mengine  mengi ambayo anasema hawezi hata kuhadithia. 

Ukimuangalia  Moh’d  bado yale machale ya uteja  uteja anayo. Sauti  ya kulaza kidogo, mapozi yake na hata macho yake. Lakini anasema kwa sasa  ameokoka   kwani  kilevi cha aina  yoyote kwake ni sawa na mkwe !

‘’’Ni baadhi ya athari tu za matumizi ya mambo  kwa muda mrefu, Mungu keshaniokoa na balaa zile tena braza ‘’ Anasema na  kuongeza kwamba,  ‘’Baada ya kufukuzwa jeshini niliingia  mtaani, vijiwe vya pombe na matumizi ya dawa za kulevya ndio vyangu. Enzi  zangu mie, mkulima  sikuchagua jembe; bia, gongo, bangi, cocaine na mengine twende kazi tu. Na hayo ndio yalionichanganya  zaidi’’ Anasimulia Moh’d. 

Aaa !  za mwizi ni arobaini. Baada ya  chatu kumeza vinavyomezwa na visivyo vya  kumeza, mkono wa sheria ulimkamata chatu kwa kosa  la  kuvunja  na kuiba kwa kutumia nguvu. Kosa hili lilitosha kwake kufungwa kwa kipindi cha miaka  mitatu kuanzia mwaka 2004 - 2006. 

Maisha ya   jela ni ya uchungu na hadithi  za kusadikika  anasema Moh’d. Lakini kama kuna kitu ambacho amejifunza katika kipindi hichi ni kuishi bila matumizi ya dawa za kulevya. 

‘’Siku za mwanzo zilikua adha kubwa sana kwangu pale  jela. Si unajua tena uteja. Kama umezoea kupasha ukikosa tu mgonjwa. Niliumwa sana lakini baadae  nilizoea kuishi bila ya kutumia dawa za kulevya  na akili na mwili wangu  ukarudi’’  Anasimulia, 

Safari ya chuo cha mafunzo kwa  Moh’d  iliishia  mwaka  2006. Lakini jee chuo cha mafunzo kilimfunza nini?. Jee kilimfanya kuwa raia  mwema? Ile nidhamu na kuheshimu   wanayotaka wakubwa ilibakia  moyoni mwake. Ataacha kumeza alivyomeza kama chatu? Jee  kipindi cha kukaa  jela   bila ya kutumia dawa za kulevya kilitosha kumfanya aache kutumia dawa hizo? La  hasha na la haula !

‘’Baada ya kutoka jela nilijihisi  kama nimechanganyikiwa zaidi. Dunia iliniinamia tena. Sina kibarua. Familia  inaniangalia. Sijui nianze wapi nitokee  wapi ili nipate  tonge ya  siku. Nilikutana na rafiki zangu  wale wale.Sikuwa na kazi ya kufanya. Nikarejea  maisha ya vijiwe  na nikaanza kutumia  tena  dawa  za kulevya’’  Anasimulia  Moh’d.


Katika  kipindi  hichi Chatu alirejea  uchatu wake. Na mnamo  mwaka  2008  akashtakiwa kwa kosa la kuvunja  na  kuiba  na kufungwa tena  jela  kwa miezi  mitatu. 

Kama kuna kitu kilichangia  na kumuuma sana kisaikologia  basi ni familia yake.Kwani katika kipindi chote hichi  cha  mawimbi ya dharuba ndani ya maisha yake basi Moh’d alikua na  familia. Mnamo mwaka  1994  akiwa mwanajeshi alioa na Mungu alimbariki watoto wa nne.

‘’Yaani mwanangu alikuja na kunieleza huku akilia’’ Anasimulia 

‘’Hebu  baba  acha tena mambo haya. Sisi hatuna raha. Si skuli  si nyumbani na watu wanatuambia baba yenu  ‘levi’  vuta unga   na ni mwanachama wa jela’’ Alisema  Pamoja na kwamba yeye binafsi alichoshwa  na maisha haya lakini msukumo wa familia ulimsogeza  zaidi juu ya kuwa na ari ya  kubadilika 

Mnamo  mwaka  2009, Mohd au Chatu alijiunga na Sober  house ya Miembeni   kwa kipindi  cha miezi minne .Kwa sasa kituo hicho   kipo   Bububu. Lengo ilikua   ni kutafuta mbinu za kuacha kabisa matumizi ya dawa za kulevya.

Si haba baada ya kukaa hapo kwa muda  wa miezi  minne na kupatiwa ushauri  nasaha, matibabu na kujengwa kisaikolojia basi nuru ya maisha yake ilirudi tena.

‘’Nilianza kubadilika, kiakili  kimwili na nikawa na mtazamo wa kuionyesha jamii kwamba nimebadilika ‘’. Anasema Moh’d. 

Moja   ya changamoto ambazo alipambana nazo  mara ya baada ya  kumaliza  Sober ni kurejesha  heshima yake  katika  jamii. Kuivua sura ya Chatu  na kuirejesha  heshima ya  jina lake tukufu  yaani Muhamad. 

‘’Haikua rahisi. Hata nilipokwenda  kuwatembelea jamaa zangu walihakikisha hawaniachi peke yangu ukumbini. Walidhani bado ni kama yule chatu wa zamani. Wa kuondoka na hata toise  za  watoto  za ukumbini’’. Anasimulia kwa masikitiko. 

Mwaka  2010, Moh’d alihamia Pemba. Bado msukumo wa kusaidia wenzake ambao bado wamo katika dimbwi la athari za dawa za kulevya ni kiu  iliyobakia moyoni mwake. 

Kwa   kushirikiiana na wana Jumuia ya Kudhibiti matumizi ya Dawa za Kulevya na Mimba za Umri mdogo yaani  JUKAMKUM  walianzisha kituo Pemba. Lengo  la kituo hicho  ni kuwasaidia  vijana ambao wamepigika na matumizi ya dawa za  kulevya  kwa lengo  la kuwasaidia kufanya  marekebisho ya tabia. 

Moja kati ya mafanikio ambayo anayaeleza kwa sasa  ni kwamba heshima yake imerudi, jamii inamkubali na amefanya  mengi ya kutunukiwa hata tunzo kwa kuwaokoa  vijana waliopita katika  mkondo wa maisha aliopita. 

Hadi hii leo, kituo cha Sober  kilichopo mkoroshoni Pemba kimechukua vijana waliothirika na matumizi ya dawa za kulevya    wapatao  97.  Miongoni  mwao ambao wamebadilika kama yeye ni  37. Wameacha kabisa kutumia dawa za kulevya na ni vijana ambao kwa sasa wanachapa kazi na kusaidia  familia  zao.

‘’Najisikia faraja  sana nikiwaona washkaji zangu ambao tulipigika pamoja kwamba tunawatoa katika hali  ile ya hatari na  sasa wameacha  kabisa.’’

‘’Mimi ni mfalme sasa, mimi ni milionea. Si wa pesa wala nini, ni mileonea ninaeishi  bila ya kutumia  dawa za kulevya kama zamani. Huu ni utajiri  wangu, kujiona kwamba nakubalika na nasaidia familia yangu ambayo  pale zamani ilinikataa kabisa’’  Anasema kwa furaha Moh’d. 

Kwenye  mafanikio hakukosi changamoto. Moh’d anatoa mawazo yake ya kuhitimisha makala haya kwa kusema . 

‘’Sober  zipo  na zitaendelea  kuwepo. Lakini boss  wangu  sisi tunakata tawi  tu, vigogo na mashina na mizizi ipo na inajulikana. Tawi litachipua na majani mengine yataota. Lakini wapo ambao wanaweza kukata mizizi na hili linajulikana. Tukiikata mizizi sober zitakosa kazi na mimi nitafurahi sana kwani tutaishi bila ya vijana kutumia  dawa za kulevya .Lakini kwa sasa ……..’’ Hakuongea kitu tena, alitikisa kichwa huku akinisimulia hatari iliyopo ya uingizwaji  na utumiaji wa dawa  za kulevya . 

Kwa  sasa Moh’d  si Yule  tena wa kutembea barabararani bila hata yebo  yebo. Vijana wanasema si Yule  wakuongea  utadhani  domo linaujauzito.Yuko safi, mtanashati na kimbilio la vijana ambao wanahitaji msaada wa hali na mali ili kujitoa  kwenye balaa ya matumizi  ya dawa za  kulevya. 

Waswahili  wanasema, papo kwa papo  kamba hukata jiwe. Elimu ya ushauri nasaha imemsaidia  Mohamed. Mwisho anasimulia  

‘Bado wananiita Chatu,  sikatai ni utambulisho  na umaarufu wangu. Lakini si Chatu wa kumeza mbuzi au hata  paa. Kama ni Chatu  ni yule anaetumika kucheza ngoma  ya Kibisa; sitafuni wala  sikangati. Ni kimbilio na faraja kwa walioathirika na matumizi ya  dawa za kulevya‘’  

“ Eti, wananiita bosi sasa. Si unaona  ‘’ Anamalizia na kunifahamisha kwamba kwa sasa  yeye  ndio Manager wa Sober House iliyopo  Mkoroshoni Pemba. 

CDC.jpgCHAI.jpgGlobal Fund Logo.pngLOGO ONE UN.jpgPEPFAR.pngUNAIDS.jpgUNDP.jpgUNFPA.jpgUNICEF.pngUSAID.jpgWHO.pngWORLDBANK_LOGO.jpg